Kiswahili

Mwongozo 1 kati ya 5 · Utambuzi

Dalili za ugonjwa wa kusahau

Takriban dakika 3 kusoma · Ulikaguliwa Septemba 2026

Mambo makuu

  • Dalili za mapema ni pamoja na kusahau matukio ya karibuni, kupotea, na kupata shida na kazi za kila siku.
  • Hisia na tabia zinaweza kubadilika pia.
  • Ukiona dalili hizi, mtu huyo anapaswa kumwona mhudumu wa afya.
  • Magonjwa mengine yanaweza kuleta dalili zinazofanana, na baadhi yake yanatibika.

Mabadiliko ya kuangalia

Kila mtu husahau mambo wakati mwingine, lakini ugonjwa wa kusahau ni zaidi ya hivyo. Angalia mabadiliko yanayojirudia na kuzidi kwa miezi. Mabadiliko haya hutokea kwa sababu ugonjwa huathiri kumbukumbu, kufikiri na uamuzi. Mtu anaweza:

  • kusahau mambo yaliyotokea hivi karibuni
  • kupoteza au kuweka vitu mahali pasipofaa
  • kupotea, hata mahali anapopafahamu vizuri
  • kusahau siku, mwezi au mwaka
  • kupata shida kufuata mazungumzo au kupata maneno sahihi
  • kushindwa kufanya kazi alizokuwa akizifanya kwa urahisi, kama kupika au kushughulikia pesa
  • kupata shida kufanya maamuzi au kutatua matatizo
  • kushindwa kukadiria umbali au ngazi

Mabadiliko ya hisia na tabia

Ugonjwa wa kusahau unaweza kubadilisha jinsi mtu anavyojisikia na anavyotenda, si kumbukumbu tu. Mara nyingi familia huona mabadiliko haya kabla ya matatizo ya kumbukumbu. Hii ni kwa sababu ugonjwa pia huathiri sehemu za ubongo zinazodhibiti hisia. Mtu anaweza:

  • kuwa na wasiwasi, huzuni au hasira kuhusu kumbukumbu yake
  • kuonekana kama mtu tofauti
  • kutenda kwa njia zisizo za kawaida kwake
  • kuacha kuwaona marafiki, au kuacha mambo aliyokuwa akiyafurahia

Muhimu: kuchanganyikiwa ghafla

Kuchanganyikiwa ghafla kwa kawaida si ugonjwa wa kusahau. Mtu akichanganyikiwa ndani ya saa chache au siku chache, inaweza kuwa ni maambukizi au ugonjwa mwingine. Matatizo haya yanaweza kuwa makubwa haraka, lakini mara nyingi yanatibika. Tafuta msaada wa matibabu mara moja.

La kufanya ukiwa na wasiwasi

  • Andika unachokiona. Andika kilichotokea na lini.
  • Zungumza na mtu huyo kwa upole. Huenda naye ana wasiwasi.
  • Nenda naye kwa mhudumu wa afya. Zahanati au hospitali ni mahali pazuri pa kuanzia.

Si kila tatizo la kumbukumbu husababishwa na ugonjwa wa kusahau. Maambukizi, upungufu wa vitamini, matatizo ya tezi ya shingo, sonona na madhara ya dawa yanaweza kuleta dalili zinazofanana. Mengi ya haya yanatibika yakigunduliwa. Ndiyo sababu kuchunguzwa ni muhimu.

Soma mwongozo unaofuata: kuchunguzwa na mhudumu wa afya

Mwongozo huu unatoa taarifa za jumla kuhusu ugonjwa wa kusahau. Si ushauri wa kitabibu kwa mtu mmoja mahususi. Daktari, muuguzi au mhudumu wa afya anayemfahamu mtu huyo anaweza kutoa ushauri unaomfaa. Tafadhali zungumza naye kuhusu wasiwasi wowote.

Ukurasa huu umetafsiriwa kutoka Kiingereza. Toleo la Kiingereza ndilo la msingi. Soma kwa Kiingereza